Jinsi aibu ndogondogo za Kenya Airways, JKIA zinavyochoma picha kwa nchi isiyohitaji stakabadhi ya viza
NA WANDERI KAMAU
MATATIZO ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), jijini Nairobi, yameibua maswali kuhusu ikiwa Kenya iko tayari kutekeleza mpango wa kuondoa hitaji la stakabadhi ya viza kwa wageni wanaowasili nchini kutoka nchi za nje.
Kwa miaka michache iliyopita, JKIA pamoja na Shirika la Kenya Airways (KQ) zimekuwa zikiandamwa na kila aina ya matatizo.
Kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita, KQ imekuwa ikipata hasara ya mabilioni ya pesa karibu kila mwaka, licha ya juhudi za serikali kujaribu kuisaidia kuanza kupata faida.
Ni hali ambayo kwa wakati mmoja ilizua ghadhabu miongoni mwa Wakenya, kwamba serikali ilikuwa ikielekeza mabilioni ya fedha katika shirika hilo, licha ya juhudi hizo kutozaa matunda.
Kando na shirika hilo, msururu wa matatizo umekuwa ukishuhudiwa katika uwanja wa JKIA, hali ambayo imezua tashwishi kuhusu ikiwa Kenya itafaulu kutekeleza mpango wa kuwaruhusu raia wa kigeni kuingia nchini bila viza kuanzia mwaka 2024, kama alivyoahidi Rais William Ruto wakati wa sherehe za Sikukuu ya Jamhuri mnamo Desemba 12, 2023.
Kulingana na wataalamu wa masuala ya kiuchumi, matatizo hayo yanahatarisha mustakabali wa KQ, ikiwa serikali haitachukua hatua za haraka kulainisha baadhi ya matatizo yaliyopo.
“Shirika la KQ lilikuwa linasifika sana katika miaka ya 1990 na 2000 kutokana na ubora wa huduma zake. Lilikuwa kwenye ligi moja na mashirika mengine ya ndege duniani kama vile Lufthansa, Panama, Delta, KLM kati ya mengine. Hata hivyo, matatizo yanayolikumba yanazua hofu kuhusu ikiwa liko tayari kuwapokea watu kutoka kote duniani kuanzia Januari, ikiwa serikali itafutilia mbali hitaji la viza,” asema Bw James Shikwati, ambaye ni mtaalamu na mdadisi wa masuala ya kiuchumi.